Imesema imefikia hatua hiyo kutokana na gazeti hilo kukiuka maadili ya uandishi wa habari mara kwa mara.
Hilo ni gazeti la pili kukutana na kifungo hicho ndani ya muda mfupi baada ya gazeti la CCM, Uhuru kufungiwa kwa siku 14 kwa kosa la kuandika habari yenye kichwa cha habari “Sina wazo kuwania Urais 2025 – Samia” inayodaiwa kupotosha kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan alipohojiwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC).
Taarifa iliyotolewa leo, Septemba 5,2021 na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari, Gerson Msigwa imesema gazeti hilo limekiuka masharti ya leseni liliyopewa, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuhatarisha usalama wa nchi kwa kuleta chuki miongoni mwa jamii na kuwafanya wananchi waichukie Serikali na viongozi wake.
“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 9(b) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016 nimeamua kusitisha kwa muda wa siku thelathini (30) leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la Raia Mwema kuanzia kesho tarehe 06 Septemba, 2021,” imesema Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali.
Amesema uamuzi wa kusitisha leseni ya gazeti la Raia Mwema unatokana na mwenendo na mtindo wa uandishi wa habari na makala ambao kwa kiasi kikubwa unakiuka misingi ya maadili ya taaluma ya habari kwa kufanya upotoshaji wa mara kwa mara wa taarifa na uchochezi wa bayana.
“Mifano michache ya habari na makala ambazo kwa kiasi kikubwa zilikiuka masharti ya leseni, misingi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ni pamoja na gazeti toleo Na.844 la tarehe 21 Agosti, 2021 lililochapisha habari iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Maumivu mapya 17”.
Taarifa hiyo imeeleza kwua katika habari hiyo gazeti lilikwenda kinyume na vifungu vya 52(1) (a), (c), (d) na (e) pamoja na 54(1) vya Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016 kwa kuchapisha na kusambaza habari zinazoleta taharuki miongoni mwa jamii na wananchi kwa kuonyesha Serikali inawaletea maumivu wananchi kwa kuweka tozo 17 za kazi mbalimbali za wasanii.
“Kana kwamba hiyo haitoshi, gazeti la Raia Mwema toleo Na.853 ukurasa wa 1 na kuendelea ukurasa wa 3 na wa 4 liliandika habari yenye kichwa kisemacho “Hamza wa CCM hatari,”. Kwanza kwa kuonekana dhahiri kukosa weledi na udanganyifu gazeti hili lililotolewa Septemba 3, 2021 liliandikwa limetolewa tarehe 3 Agosti, 2021 na katika habari hiyo linawanukuu watu wawili lililowaita Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Manumba, mara linamtaja DCI Wambura.
Msigwa kupitia taarifa hiyo amesema ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari inaamini adhabu hiyo itawapa nafasi ya kuboresha masuala yanayohusu weledi wa uandishi wa habari na utekelezaji wa masuala yote yanayohusu uzingatiaji wa Sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya habari.
Ameongeza kuwa ikiwa wahusika hawataridhika na uamuzi huo wana haki ya kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana ya habari ndani ya siku 30 tangu siku ya uamuzi huo.
0 Comments