Ofisi ya Makamu wa Rais imesaini Mkataba wa Shilingi Bilioni 18.8 na
Kampuni ya ujenzi ya SUMA JKT wa kuanza awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi
ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Hafla ya kusaini Mkataba wa ujenzi huo imefanyika katika Ofisi ya Makamu
wa Rais Mtumba jijini Dodoma Oktoba 13, 2021 na kukabidhi rasmi eneo la
ujenzi kwa Mkandarasi baada ya kushinda zabuni, na kushuhudiwa na
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambaye ndio Msimamizi Elekezi wa ujenzi
wa jengo hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi.
Mary Maganga ameipongeza SUMA JKT kwa kushinda kandarasi hiyo na kutaka
ujenzi uwe wa haraka kwa kuzingatia ubora, viwango na kasi.
“Ninaamini kuwa SUMA JKT mna uzoefu mkubwa, na ujenzi huu utaenda kwa
kasi, na kuzingatia viwango vya ubora wa hali ya juu, na ikiwezekana
mkamilishe kazi hii kabla ya muda uliopangwa,” amesema Bi. Mary Maganga.
Aidha, Katibu Mkuu alisema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza ufanisi
katika utekelezaji wa majukumu kwa kuwa Serikali ilipohamia Dodoma jengo
lililojengwa katika eneo la Mtumba halitoshelezi mahitaji ya watumishi
wote hivyo kulazimika kutumia jengo lingine mjini kwa ajili ya watumishi
wa idara zingine.
“Wenzetu wa Idara ya Mazingira wapo wengi na wana majukumu mengi kila
tunapowahitaji kuja kwa ajili vikao inabidi waje huku Mtumba kwa hiyo
jengo hili likikamilika ndani ya muda tuna imani ufanisi utaongezeka na
tunaweza kufanya kazi kwa pamoja na muda tunaotumia barabarani utapungua
au kuondoka kabisa,” alisema.
Aidha, Bi. Mary Maganga amesema, msimamizi wa ujenzi huo Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) atafanya kazi kwa karibu na Kamati ya Ujenzi ya
Ofisi ya Makamu wa Rais inayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Bw. Mohammed
Khamis Abdullah na kusisitiza kutenga Ofisi kwa ajili ya Ofisi ya
Uratibu wa Shughuli za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Ofisi ya Makamu wa Rais ndio wasimamizi wa Masuala ya Muungano na
Mazingira hapa nchini, hivyo tutatoa nafasi katika jengo hili jipya kwa
ajijli ya wenzetu wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali kwa upande
wa Zanzibar kupata nafasi ili kurahisisha masuala ya uratibu wa
utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa pande zote mbili za Muungano.”
ameongeza Bi. Mary Maganga.
Naye, Mhandisi Morgan Nyonyi kutoka SUMA JKT amemthibitishia Bi. Mary
Maganga kuwa, SUMA JKT watatekeleza mradi huo kwa ustadi mkubwa kwa
kuhakikisha wanakailisha mradi huo wa ujenzi kwa wakati na ikiwezekana
kabla ya miezi 24 iliyopo ndani ya Mkataba.
“Tutajitahidi kwenda na wakati na kuzingatia viwango vya ubora,
rasilimali fedha na rasilimali watu tunao wa kutosha. Naishukuru
Serikali kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha zitakazowezesha kutekelezwa
kwa mradi huu na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutuamini SUMA JKT”
Alisisitiza Mhandisi Nyonyi.
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma za Kihandisi wa NHC, Mhandisi Manning
Mwalaka, amesema Shirika litahakikisha Mkandarasi anafuata taratibu zote
za ujenzi kwa mujibu wa mkataba katika kipindi chote cha utekelezaji wa
mradi.
“Sisi na NHC tumepewa dhamana ya kuwa wasimamizi katika mradi huu,
tutashirikiana kwa pamoja, na kuhakikisha kwamba hili jengo linajengwa
kwa viwango vilivyokusudiwa,” ameeleza Mhandisi Mwalaka.
Kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo, kutapelekea Idara na Vitengo vyote vya Ofisi ya Makamu wa Rais kuhamia katika jengo hilo.
0 Comments