ELIMU YA FEDHA:
Kwenye maisha kuna mstari usioonekana (invisible line) ambao unawazuia watu wengi sana.
Wakati mwingine mstari huu unachorwa kwenye familia nzima, kuna kiwango fulani cha pesa ambacho hakuna mtu katika hiyo familia huwa anaruhusiwa kukipata.
Ni kama vile kila mtu anatakiwa kuishia kwenye kiwango fulani tu.Utashangaa kila ambaye anakaribia “kutoboa” na kuanza kufanikiwa, kuna kitu kinatokea ambacho hakikutarajiwa na kila kitu kinaanza kwenda mrama.
Wakati mwingine mstari huu unakuwepo kwenye kundi la marafiki, unakuta wote kipato chenu hakivuki kwenye kiwango fulani.
Wakati mwingine mstari huu huwa kwenye ofisi fulani au kwenye taaluma fulani.
Umeshawahi kuwa katika hatua fulani ya maisha yako halafu unaona kabisa unakaribia kupata mafanikio ya kifedha lakini hayaji tena?
Unakumbuka ulipokuwa unadhani ukipata kiwango unachokipata sasa hivi mambo yatakuwa mazuri ila baada ya kuanza kupata ni kama maisha yako vilevile?
Kuna wakati uliamini msharaha ukipanda, ukipata kazi mpya, ukipata mtaji zaidi au ukipata mkopo mambo yatabadilika kwa haraka?
Makala hii ni kwa ajili ya watu ambao wamechoka kuwa katika kiwango kilekile cha kifedha na wanatamani kuvuka mstari ambao wamekuwa wanashindwa kuuvuka siku nyingi katika maisha yao.
Watu ambao wanatamani kuishi juu ya mstari wa wastani, watu ambao wanasema “Niko tayari kuzijua siri muhimu za kifedha na kuanza kuziishi mara moja”. Kila wakati niko kwenye madeni, bili zimejaa na zinanisumbua, kila wakati kipato changu hakitoshi.
Nifanye nini?
Ni kweli napata pesa ya kunisaidia kulipa gharama za kawaida za maisha, ila ninachopata hakiwezi kunisaidia kufanya mambo makubwa ninayotaka maishani, ni kweli sihangaiki nina uhakika wa kipato changu, ila hakikui kwa kasi kama ninavyotaka, hivi ninaweza je kufanya kipato changu kiwe kikubwa zaidi ya sasa hivi?
Kama umewahi kujiuliza moja ya maswali haya. Basi kitabu hiki ni kwa ajili yako.
Hongera sana unapovuka mstari ambao wengi umewazuia, karibu kwenye maisha juu ya wastani!
KUJENGA MTAZAMO NA UFAHAMU
CHANYA KUHUSU FEDHA
"Kuna Siri kubwa sana kuhusu saikolojia ya pesa. Watu wengi hawaijui na ndio maana wengi wameshindwa kupata mafanikio ya kifedha. Kukosa fedha sio tatizo, bali ni ishara kuwa kuna kitu hakiko sawa ndani yako”
T.HARV EKER (Rais wa Peak Potentials Training)
Lengo: Somo hili linakusudia kukusaidia kukupa ufahamu sahihi kuhusu mafanikio ya fedha na jinsi ya kujuhakikishia kuwa unapata uhuru wa kifedha katika maisha yako.
Jambo lolote katika maisha yako ili litokee linahitaji kuhusisha mabadiliko ya ufahamu na akili yako, vilevile mabadiliko ya kifedha na kipato yatahusisha pia mabadiliko ya mitazamo na namna ambavyo unafikiri.
Mafanikio ya kifedha huanza na ufahamu wako wa kifedha.Kwa kawaida kuna hatua zifuatazo ili uweze kufanikiwa katika eneo la fedha:
- Amua kwa ufasaha unachotaka.
- Amini kwamba inawezekana na unastahili kufanikiwa kifedha.
- Uwe makini kila siku kufanikisha malengo yako.
- Uwe tayari kuwa na nidhamu na kulipa gharama zinazohitaji hebu tuanze kuangalia hatua hizi kwa ufasaha sasa.
- AMUA KWA UFASAHA UNACHOTAKA
Hakuna mtu ambaye anafanikiwa kwa bahati.
Kila ambaye amefanikiwa katika maisha yake basi ujue kuna siku aliamua kuwa vile alivyo leo. Kwa ufupi ni kuwa mafanikio yetu ni matokeo ya maamuzi yetu.
Kinachoshangaza ni kuwa watu wengi sana hawajawahi kuamua kwa ufasaha kwenye eneo la kifedha wanataka kuwa na mafanikio ya namna gani.
Ni rahisi sana kusikia watu wanasema nitasoma hadi niwe na degree ama nitaoa na kuwa na watoto watano lakini ni mara chache sana kusikia watu huwa wanapanga kiwango cha mafanikio yao kifedha.
Hebu na wewe jiulize umeshawahi kukaa chini na kuamua kiwango gani cha mafanikio yako ya kifedha ambayo unayataka kwenye maisha yako?
Umeshawahi kuamua unataka kuwa na utajiri wa kiasi gani baada ya miaka 10?
Umeshawahi kuamua kipato chako cha mwaka huu kiongezeke hadi kiasi gani?
Kama umejigundua kuwa haujawahi kuwa na mpango thabiti juu ya kiwango cha mafanikio yako ya kifedha ambayo unayatafuta basi ujue umeshaingia katika kundi la watu ambao watachelewa sana kufanikiwa kifedha.
Tumia muda wako leo na uandike kwa ufasaha unataka kuingiza kiwango gani cha fedha kwa kila mwezi wa mwaka huu, kwa mwakani, miaka 10 n.k
Hatua hii ni muhimu sana kwani unaupa taarifa ubongo wako kujiandaa kukupatia mawazo ya kukusaidia ili uweze kutengeneza kiwango cha fedha ambacho kinahitajika.
2. AMINI KWAMBA INAWEZEKANA NA UNASTAHILI KUFANIKIWA KIFEDHA
Kuna watu wengi sana kwa sababu mbalimbali wamejikuta wako kwenye fikra za kutokuamini kuwa wao wanaweza kufanikiwa kifedha katika maisha yao.
Mara nyingi sana hii huwa inajidhihirisha kwa ndani ingawa kwa nje wanaweza wasiionyeshe kabisa.
Hata wewe unavyosoma kuhusiana na somo hili la fedha inawezekana ndani yako umejiwekea ukomo wa mafanikio yako ya kifedha na unaamini kuna watu maalumu ambao wanaweza kufanikiwa ila sio wewe.
Hii imetokana na mazingira ya ukuaji wetu katika familia na na jamii zetu. Kuna wengi ambao wamekulia katika mazingira ambayo wazazi wao walikuwa wanawaonyesha kuwa pesa ni kitu kigumu sana.
Walikuwa wakiomba pesa wanajibiwa “Unafikiri pesa zinaokotwa?”. Kasumba hii wamekuwa nayo na wanaamini kuwa hakuna namna wanaweza kupata pesa kwa sababu huwa haipatikani kabisa.
Na kwa sababu ubongo wao umeamini kabisa hili, wameshindwa kabisa kuamini kama wanaweza kufanikiwa.
Kuna wengine wameaminishwa mafanikio ya kifedha ni kitu kibaya sana na kila aliyefanikiwa ni muovu.
Hawa ni wale walipokuwa watoto walikuwa wanaambiwa “Usimuone amefanikwia yule, ni mwizi au ameua mtoto wake".
Hii wamekuwa nayo na ndio maana kila aliyefanikiwa huwa wanamuhusisha na jambo lisilo la kawaida, utasikia “Ni Freemason, ameua, ameiba n.k".
Ingawa wapo watu ambao wanatumia njia hizi kwenye maisha yao ila ukweli ni kuwa wapo wengi pia ambao wamefanikiwa kwa kutumia kanuni za kawaida kabisa ambazo na wewe unaweza kuzitumia.
Watu wa namna hii ndio wale utakuta wanaishi kwenye shida, madeni na changamoto ya kifedha na hawataki kujifunza na huwa na misemo yao:
- Fedha ni dhambi.
- Watu wenye fedha ni wabinafsi.
- Ukiwa tajiri hauwezi kumcha Mungu.
- Hata uwe bilionea hauwezi kununua furaha
- Kila mtu hawezi kufanikiwa kifedha kuna wachache tu wameandaliwa n.k
Hii yote ni kuonyesha kuwa hawaamini kama WANAWEZA na Hawaamini kama wanastahili.
Je, na wewe ni mmoja wa watu ambao una fikra za namna hii kuhusiana na fedha?
3. UWE MAKINI KILA SIKU KUFANIKISHA MALENGO YAKO
Baada ya kujiwekea malengo na kujenga imani na kuona kuwa na wewe unaweza kufanikiwa katika kile ambacho unakifanya, hatua inayofuata ni wewe sasa kila siku kuwa makini ili uweze kutumia fursa na watu unaokutana nao ili uweze kufanikiwa katika kupata kiwango cha pesa unachokihitaji.
4. UWE TAYARI KUWA NA NIDHAMU NA KULIPA GHARAMA ZINAZOHITAJIKA.
Moja ya changamoto kubwa ya watu wengi ni kutaka mafanikio ya kifedha bila kuwa tayari kulipa gharama zinazohitajika.
Kuna mambo ambayo ukianza kuyafanya kwenye maisha yako utaanza kupata mabadiliko makubwa sana kwenye eneo la fedha tofauti kabisa na ambavyo ulivyo sasa.
Moja ya gharama unayohitaji kuilipa ni kupata ufahamu kuhusiaana na mambo ya fedha. Kitu kimojawapo kinachoshangaza sana ni kuwa, ingawa huwa tunatumia pesa kila siku na huwa tunazihitaji kufanikisha ndoto zetu, katika masomo yetu shuleni huwa hatufundishwi kabisa kuhusiana na fedha na tabia zake ili tuweze kuhusiana nayo kwa mafanikio.
Ili kufikia mafanikio ya kifedha ni lazima kujenga nidhamu muhimu ambayo inahitajika ili tuweze kupata kile amnacho tunakitaka.
ZOEZI
1. Tumia muda kutafakari na kujiuliza kama una malengo thabiti ya kifedha katika maisha yako.
Kama bado hauna tumia muda kidogo kufikiria kuhusu mafanikio yako ya kifedha.
Kama bado hauna tumia muda kidogo kufikiria kuhusu mafanikio yako ya kifedha.
- Kiwango unachotaka kutengeneza kwa mwezi
- Mwaka huu kipato chako unataka kiwe kimeongezeka kwa kiwango gani
- Wakati unapostaafu unataka kuwa na utajiri wa kiasi gani?
- Miaka 10 tangu sasa unataka kuwaje katika eneo la kifedha?
KANUNI YA DHAHABU YA MAFANIKIO YA KIFEDHA.
“Ili uweze kufanikiwa katika eneo la kifedha, ni lazima uweze kujenga mkakati wa maana na wa kudumu utakaouheshimu kila wakati"
Ni kukusaidia kujua kanuni ya kwanza ambayo imewahi kutumika na watu mbalimbali na ikawasaidia kufanikiwa kutimiza malengo yao kifedha.
Moja ya changamoto muhimu sana ambayo lazima mtu yoyote akabiliane nayo ni uwezo wa kuweka sehemu ya kila pesa ambayo anaipata kwenye akiba maalumu ambayo inaweza kumsaidia hapo baadaye kufanya kitu maalumu na kitu kikubwa zaidi.
Kati ya kanuni nyingi za kifedha ambazo unaweza kuzifahamu kwenye maisha yako, kuna kanuni moja ambayo ni ya muhimu sana katika kukuhakikishia mafanikio yako ya kudumu ya kifedha.
Kanuni hii imeelezwa na wataalamu wengi kuwa ndio hasa msingi mkubwa wa mafanikio yako ya kifedha. Kati ya wakufunzi wakubwa ambao wameitaja kanuni hii kama ndio msingi wa kifedha ni:
George Clason kwenye kitabu chake cha “THE RICHEST MAN IN BABYLON”
Jack Canfield kwenye kitabu chake cha “THE PRINCIPLES OF SUCCESS”
Makala maalumu ya gazeti la Forbes kuhusu namna ya kutengeneza utajiri.
Robert Kiyosaki, David Basch Kwenye kitabu chake cha AUTOMATIC MILIONAIRE
Sio kanuni ya ajabu ila huwa inaleta Maajabu.
Kanuni hii rahisi sana kuisikia ila imekuwa ngumu sana kwa wengi kuitekeleza, huwa inaitwa “JILIPE WEWE MWENYEWE KWANZA” (Pay yourself first).
Kanuni hii inakutaka kila unapopata pesa kwenye maisha yako, utenge sehemu ya pesa yako ambayo utaihifadhi kwa ajili ya matumizi yako ya kimkakati ya baadaye.
Hii inamaanisha kuwa kabla haujaanza kulipa bili zako,kununua nguo ama chochote kile, hakikisha kuwa unajilipa sehemu ya pesa unayopata.
Kama ukiweza kufanya hivi kwa miaka kadhaa utaweza kujikuta kuwa umewekeza kiasi kikubwa sana cha pesa yako na kitakusaidia kufanya mambo makubwa sana huko mbeleni.
Hebu jaribu kutafakari. Kama ungekuwa unawekeza kiasi cha asilimia kumi ya kila pato ambalo unalipata kwenye maisha yako katika akaunti maalumu kwa miaka 10 iliyopita, ungekuwa umeshakusanya kiasi gani.
Jaribu kutafakari kidogo.
Vivyo hivyo hebu jaribu kufikiria kama uataweza kuwekeza kiasi cha asiliamia kumi cha kila pesa ambayo inapita mkononl mwako miaka kumi ijayo kuanzia sasa utakuwa umeshafika wapi?
Kwa nini watu wanajua umuhimu wake ila wanashindwa kuweka?
Ni vyema kujua kuwa inawezekana hata wewe leo sio mara yako ya kwanza kusikia kuhusu kanuni hii ila haujawahi kuifanyia kazi.
Na inawezekana kabisa ukaisikia leo na ukaiacha bila kuifanyia kazi yoyote katika maisha yako. Kuna sababu kadhaa zinazowafanya watu washindwe kuiweka katika matendo kanuni hii.
Sababu ya kwanza
Watu wengi sana huwa wanasema asilimia kumi ya kipato chao ni sehemu kubwa sana na wakiitoa na kuiwekea akiba basi hawataweza kufanya bajeti yao itosheleze.
Lakini cha ajabu ni kuwa ukifuatilia hiyo asilimia kumi wanafanyia nini, wengi utakuta inaishia kwenye matumizi ambayo sio ya lazima kabisa.
Kama wewe ni mmoja wa watu ambao unafikiri hauwezi kuweka asilimia kumi ya kipato chako kama akiba ya kubadilisha maisha yako, hebu jaribu kujiuliza namna unavyotumia pesa yako. Wengi wanoshindwa ni wale ambao hata hawajui pesa yao huwa inatumikaje.
lla nashauri hata kama hauwezi kuanza na asilimia kumi kwa sasa, tafuta asilimia ndogo ambayo unaweza kuanza nayo kwa sasa hata kama ni 5% ama 1%.
Kikubwa hapa kinachotafutwa ni nidhamu yako.
Kumbuka kuwa kama leo hauwezi kuweka asilimia kumi ya kipato chako kwa sababu unafikiri ni kidogo basi ujue hata ukiongeza kipato na kikawa kikubwa hautakuwa na uwezo wa kuweka akiba pembeni.
Kinachokufanya ushindwe kuweka sio kwa sababu hauna kipato kikubwa ila ni kwa sababu hauna nidhamu ya kuweka akiba. Jenga nidhamu.
Sababu ya Pili
Ni kushindwa kuwa na malengo ya muda mrefu ya kifedha. Watu wengi sana huwa hawana malengo ya muda mrefu ya kifedha, huwa wanaishi mwezi kwa mwezi bila kuzingatia kabisa maisha yao ya baadaye.
Hivi umeshwahi kujiuliza kama ikitokea umeshindwa kuwa na uwezo wa kufanya kazi baada ya miaka kumi kutokea leo utakuwa unaishije?
Hivi kukitokea jambo abalo likakuzuia kufanya shughuli zako za kila siku, umeshawahi kuwaza utakuwa unaingizaje pesa zako?
Jifunze Jinsi ya Kuyatafuta na Kuyamiliki Maisha Bora Kupitia Mada Zetu za Saikolojia, Mapenzi, Mahusiano, Upendo, Afya, Furaha, Msaada Binafsi, Ngono, Uzazi, Tabia, Ufahamu, Akili, Msongo wa Mawazo, Kazi, Kumbukumbu na Jinsia ili ufanikiwe ni lazima ujiwekee malengo ya muda mrefu sana ya mafanikio yako ya kifedha.
Utakaposema unataka kuwa na akiba ya kifedha ya milioni 100 baada ya miaka 5 ili ufanye mradi Fulani, hii inamaanisha utajua uweke kiasi gani kwa kila mwezi ili uweze kufikia lengo lako au utumie mbinu gani za kuongeza kipato ili uzipate pesa hizo.
Kumbuka kuwa unaweza kutumia kiasi hiki unachokihifadhi ikawa kama sehemu ya kuaminisha taasisi za kifedha kukupa mkopo pia hapo baadaye.
Sababu ya Tatu
Sababu ya tatu inayowafanya watu wadharau kuweka asilimia ndogo ya pesa zao wanazozipata ili kujijengea mafanikio ya kifedha ni kudharau nguvu ya kiwango kidogo.
Nguvu iliyopo katika kuanza kidogo na naamini wewe hautakuwa mmoja wa wale ambao wanadharau mwanzo mdogo.
Inawezekana kwa leo asilimia kumi yako ni 10,000 na unaona kama vile haitaweza kuleta mabadiliko makubwa yoyote yale kama ukiweka akiba. Ila kumbuka faida mbili unazozipata kwa kuweka hata kiwango kidogo.
Moja ni kujijengea nidhamu ambayo itakusaidia hata utakapokuwa unaingiza pesa nyingi sana kwenye maisha yako basi utakuwa na nidhamu ya kujiwekea akiba.
lla pili ni nguvu ya mlimbikizano (compounding effect), hii inaleelezea kuwa kila fedha unayoitenga inageuka kuwa mbegu ambayo inaweza kuleta msitu mkubwa sana.
Mkulima anayedaharau mbegu ama kula mbegu, huwa anapata shida wakati wa njaa. Siku zote kumbuka kuwa, nguvu ya mbegu haiko kwenye ukubwa wake bali iko kwenye uwezo wake wa ndani.
Utumie njia gani?
Kuna njia mbalimbali ambazo unaweza kuzitumia kufanikisha zoezi hili:
1). Tumia makato ya benki ya kabla
Kama wewe nimfanyakazi uanweza kufungua akaunti maalumu kwa ajili ya zoezi hili na ukaweka “standing order" kwenye benki yako kuwa kila mwezi kwenye mshahara wako kinaondolewa kiasi fulani na kinapelekwa kwenye hiyo akaunti ambayo unaweza kuifanya iwe "fixed account" ambayo umeiwekea kuwa utachukua pesa baada ya muda fulani tu.
Hii itakusaidia kwa sababu itakuwa inatumia kama mfumo wa kukatwa kodi ama mafao yako kwani pesa itakuwa haifiki mkononi mwako.
2). Unaweza kutumia mifuko ya jamii.
Hata kama una mfuko wa jamii ambao mwajiri
anakulipia na wewe unajilipia, siku hizi iko mifuko ya jamii imefungua mfumo ambao unakuruhusu kuweka kiasi fulani hata kama ni kidogo kila mwezi.
Uzuri wa utaratibu huu pia ni kuwa unaweza kuweka kupitia njia ya simu lakini pia kama kipato chako sio cha kila mwezi huwa kinatokea nyakati zisizo tabirika, unaweza pia kuwa unaweka kila unapopata.
Unaweza kufuatilia kwenye mifuko ya jamii yenye mifuko ya hiari.
Vipi kuhusu Hisa, Hati fungani na Mifuko ya uwekezaji ya pamoja (Mutual Fund)?
Kumbuka pia hii unaweza kuwekeza huko ila changamoto yake ni kuwa thamani ya pesa yako inaweza kubadilika kulingana na mwenendo wa soko kwa wakati huo.
Hivyo uwekezaji huu mara nyingi unachukuliwa kama ni uwekezaji ambao unatakiwa kufanya maamuzi baada ya kujiridhisha kuhusiana na hatari zilizopo na utayari wako.
Naomba uniambie mpango wako kuhusiana na utekelezaji wa kanuni hii kwa miezi 6 ijayo. Unatarajia kuwa unaweka kiasi gani kila mwezi?
PESA ZAKO HUWA ZINAKWENDA WAPI?
“Usiniambie kitu ambacho unakithamini, wewe nionyeshe bajeti yako nami nitakuambia kitu ambacho unakithamini kwenye maisha yako” - Joe Biden
Katika somo hili utajifunza namna ambavyo unaweza kuthibiti mahali ambako pesa zako zinakwenda ili usijikute unapoteza kila unachokipata.
Moja ya changamoto kubwa sana ambayo watu wengi huwa wanakabiliana nayo katika maisha yao ni ile hali ya kujikuta kila wanapoongeza kipato chao na matumizi huwa yanaongezeka.
Matokeo yake ni kuwa kuna watu wengi sana ambao kipato chao cha leo ni mara nyingi sana ya kipato chao cha miaka iliyopita lakini bado wanashangaa haziwatoshi.
Hivi haujawahi kujiuliza huwa inakuaje hata pale ambapo kipato chako kinapoongezeka bado gharama za maisha zinakuwa hazitoshelezi kuzikabili?
Hii unatakiwa kujua kuwa hakuna wakati kwenye maisha yako pesa zitakutosha, hii ndio maana hata bilionea namba moja duniani bado anafanya bidii kuendelea kutafuta pesa na hachoki.
Kanuni ya Parkinson's kwenye masuala ya kifedha na utajiri inasema kuwa sikuzote “Matumizi hujitahidi kuongezeka ili yakutane na Mapato kila yanapoongezeka".
Na hii ndio inawasababisha watu wengi sana washindwe kupata fedha za ziada kwa ajili ya kuweka akiba ama kufanya uwekezaji wa muda mrefu. Kitaalamu ili ufanikiwe kifedha ni lazima uhakikishe kuwa unaivunja kanuni hii.
Ikimaanisha kuwa mapato yako yakiongezeka basi matumizi yako yabakie vilevile ama yaongezeke kwa kiwango kidogo kulinganisha na wastani wa mapato yako ili uweze kupata kiasi cha kuhifadhi (Mfano: Kama mapato yako yameongezeka kwa 20% inabidi ujitahidi uache matumizi yako palepale ama yaongezeke chini ya 20%).
Kama wewe kipato chako kila kinapoongezeka huwa pia unaongeza kiwango cha matumizi yako kwa kasi ileile basi hautafanikiwa kupata mpenyo wa kifedha.
Swali muhimu kwa ajili ya mafanikio ya kifedha, Pesa zangu huwa zinaenda wapi?
Watu wengi sana ukiwauliza swali hili huwa wanalijibu kirahisi sana. Utasikia huwa wanasema nakula, nalipa nyumba na kujihudumia mwenyewe.
Na wengi sana ukiwaeleza kuwa wanahitaji kuwa na ziada fulani huwa watakuambia pesa wanayopata haitoshi.
Hatua ya kwanza ya kuvunja kanuni ya Parkinson ni kuhakikisha kuwa unajua kila ambako pesa yako huwa inaenda kupitia matumizi yako.
Kuna watu wengi sana hawajawahi kufanya zoezi hili na kuna wengi hata leo hawatalifanya kwa kupuuzia na matokeo yake watabakia kama walivyo leo miaka kadhaa ijayo.
Hebu jaribu kujiuliza maswali yafuatayo:
Ninajua kila mwezi huwa matumizi yangu ni shilingi ngapi kwa ujumla?
Je huwa ninatumia kiasi gani kwa kila kipengele? Nguo,chakula,vocha,mafuta n.k
Je, kuna matumizi gani ambayo naweza kuyapunguza ama kuyaacha kabisa bila kuathiri mfumo wangu wa maisha?
Zingatia yafuatayo
Mara nyingi sana watu wanapoandika bajeti kuhusu matumizi yao huwa wanakuja kugundua kuwa matumizi yao ni makubwa zaidi kuliko kipato chao cha mwezi.
Kama wewe umegundua hivi, inamaanisha kuna mambo mawili makubwa ya kufanya ambapo usipoyazingatia basi utajiingiza katika madeni ambayo yatakuathiri sana kifedha:
i. Tafuta maeneo ya kupunguza matumizi yako. Kagua matumizi yako kwa undani na ujiulize kama yako matumizi ambayo sio ya lazima uendelee nayo kwa sasa.
Hii inamaanisha unaweza kuyaacha kabisa kwa sasa hadi baadaye ama kuyapunguza ubakize matumizi ya chini kidogo katika eneo hilo.
ii. Jitahidi kutafuta mbinu ya kuongeza kipato chako.
Kama unagundua kuwa matumizi yako yote ni ya lazima na hakuna ambalo linaweza kupunguzika inamaanisha utatakiwa kuweka jitihada katika kutafuta namna ya kuongeza kipato chako.
Watu wengi sana huwa wakifikiria juu ya kuongeza kipato huwa wanawaza kiwango kikubwa sana.
Kumbuka inapofika suala la kutengeneza pesa kitu muhimu sio unatengeneza kiasi kikubwa namna gani bali ni ule ujuzi wa kutengeza pesa ndio muhimu. Kwani ukiweza kutengeza kwa mfululizo pesa hata kama ni kwa kiwango kidogo basi itakusaidia kupata kiwango kikubwa zaidi pia.
Siku zote kuwa msingi wa kuongeza thamani ya pesa na mali ambazo unazo ni kuhakikisha unajua kila pesa yako inapoelekelea.
Moja ya tofauti kubwa ya maskini na matajiri ambayo ilielezwa kwenye kitabu cha The Millionare Next Door ilikuwa ni kwamba, matajiri wana bajeti za matumizi yao na maskini hawana kabisa bajeti za matumizi yao.
Leo unaweza kuamua kujiunga na wale ambao wako kwenye safari ya kufanikiwa kifedha kwa kuandaa bajeti yako ama ukapuuzia na kuendelea na maisha ya matumizi ya pesa bila bajeti na ukaja kujilaumu hapo baadaye.
Tumia muda wako kuandika bajeti yako ya mwezi kwa kila kila kipengele ili ujue huwa unatumia kiasi gani kwa ajili ya kitu gani.
Usikubali kuishi bila bajeti ya maisha yako.
Kama mara nyingi umeshindwa huko nyuma kutengeneza bajeti yako, safari hii usishindwe.
KABILIANA NA MAWAZO YASIYO SAHIHI JUU YA PESA
"Siku zote kumbuka kuwa mawazo yako ndio mbegu ya maneno na matendo yako. Ukitaka kuanza kupata fedha zaidi ya unavyopata kwa sasa inabidi kwanza uanze kubadilisha aina ya mawazo uliyonayo juu ya fedha”
Ni kujifunza mambo ambayo inawezekana unayaamini ili sio ya kweli kuhusu pesa na yamekuwa ni chanzo cha kukwama kwako kifedha.
Kila mtu huwa anaongozwa na aina fulani ya mawazo ambayo asipokuwa makini anaweza kujikuta yamegeuka kuwa ni kikwazo kwenye maisha yake kufika kule ambako anataka kwenda.
Mambo haya ambayo huwa tunayaamini, wakati mwingine huwa yanatokea katika maisha yetu bila sisi wenyewe kujua na tunajikuta tunakuwa na tabia ambazo hatujui tumetoka nazo wapi.
Yale tunayoyaamini kuhusu pesa huwa yanatokana na mambo mbalimbali kama vile:
- Aina ya maisha tuliyoyaona kwa wazazi wetu.
- Maneno ambayo tuliambiwa ama kusikia yakizungumzwa kuhusiana na pesa.
- Uzoefu ambao tuliupitia huko nyuma kuhusiana na pesa n.k.
Kila hatua ya maisha yetu kwa namna fulani ilihusika kutujengea mtazamo na msimamo fulani kuhusiana na pesa. Na mara nyingi tabia zetu zinaongozwa na mambo haya tuliyoyasikia na tuliyoyaona kwenye maisha yetu.
Ingawa baadhi ya mambo yanaweza kuwa ni kweli, ila kuna mambo mengi ambayo unaweza kuwa umeshayaamini na yanaoongoza maisha yako na sio kweli kabisa.
Baadhi ya mambo ambayo yanaaminiwa na ambayo sio sahihi.
Kuna watu maalumu wameumbwa kuwa matajiri.
Moja ya kosa kubwa sana ambalo unaweza kulifanya kwenye maisha yako ni kuamini kuwa wewe si mmoja wa wale ambao wanatakiwa kufanikiwa sana kifedha.
Kuna watu wengi sana ambao wameshindwa kufikia kiwango kikubwa cha mafanikio ya kifedha kwa sababu tu wameamini kuwa wao hawajaumbwa kufanikiwa.
Watu wa namna hiii huwa wanaamini kuwa kuna watu ndio wamekuja duniani kufanikiwa na wengine hata wafanyaje basi hawatafanikiwa.
Sio kweli.
Siku zote kumbuka kuwa fedha ni matokeo unayopata baada ya kufanya kitu ambacho ni cha thamani.
Hivyo basi kama utaamua kujikita katika kufanya mambo ya thamani zaidi ya unavyofanya sasa utaweza kuvutia kiwango kikubwa cha fedha kuliko kile unachovutia kwa sasa.
Hivyo njia nzuri ya kuuungana na wale waliofanikiwa ni na wewe pia kufanya kitu cha thamani zaidi. Wewe pia ni mtu maalumu, usijidharau wala usijitoe kwenye kundi la watu watakaofanikiwa.
Duniani hakuna pesa za kumtosha kila mtu.
Kuna watu huwa wanaamini pia kuwa duniani hakuna pesa za kutosha kila mtu. Hii nayo sio kweli.
Kinachotokea ni kuwa kwa sababu watu wengi huwa wanasumbuliwa na tatizo la kwanza pale juu basi kuna watu wachache ambao wanajiamini wenyewe wanakusanya pesa nyingi zaidi kuliko wengine. Unakumbuka 80/20 rule?.
Lakini hata tukisema kuwa pesa ni chache kwa nini wewe unafikiri utakuwa kati ya wale ambao hawana badala ya kufikiria kuwa katika wale ambao wanazo?
Bidii yako katika kile unachokifanya ndio nguzo muhimu ya kukupa kiwango kikubwa unachohitaji. Watu wanaoamini kuwa pesa huwa hazitoshi ndio ambao hukata tamaa na kuamua kutofanya bidii ya kuendelea mbele zaidi
Hivi unajua kuwa kila siku pesa huwa zinabadilisha mikono? Hii ndio maana kila siku kuna watu wanazidi kutajirika na kuna ambao wanazidi kuwa maskini. Hii ni kwa sababu Hakuna mtu mwenye hati miliki ya pesa, bali yenyewe huenda kwa yoyote Yule ambaye anatumia mbinu sahihi.
Na wewe pesa zako ziko mahali, endelea kuzitafuta. Utazipata, ziko za kutosha.
- Ili uonekane kuwa una pesa basi ishi maisha ya anasa. Hii ni moja ya tatizo kubwa ambalo watu wengi wamekutana nalo. Watu wengi sana wanaishi kwa kutaka kuonyesha kuwa wao wana pesa kwenye maisha yao bila kujali ukweli halisi unaowakabili.
Hata hivyo utafiti uliofanywa na watu kadhaa akiwemo Prof. Stanley Danko aliyeandika kitabu cha “The Millionaire Next Door" ameonyesha kuwa matajiri wengi maisha yao wanayoishi ni ya kawaida sana kwani huwa hawaishi ili waonekane wanapesa bali wanaishi ili wapate pesa zaidi (they don't live to LOOK rich but they live to BE rich).
Kila siku maisha huwa yanakupa machaguo ya kuamua kuhusu hatima yako. Uamue kutumia poesa kwa namna ya kuonekana leo na kesho uteseke ama uamue kutumia kwa hekima leo ili kesho uishi maisha mazuri.
Nikiwa na pesa nyingi sitakuwa na Madeni.
Jambo lingine ambalo watu huwa wanaliamini kuhusu pesa na huwa halina ukweli kabisa ni kufikiri kuwa wakiwa na pesa nyingi, mshahara mkubwa ama kutengeneza faida kubwa basi hawatakuwa na madeni kabisa.
Sio kweli.
Kumbuka sababu ya kuwa na madeni sio kwa kuwa na kipato kidogo bali ni kukosa nidhamu na aina ya maisha yaliyo sahihi.
Nikuulize swali, Hivi mtu ambaye ana kipato cha 500,000/= na ana deni la 1,000,000/= ana tofauti gani na mtu ambaye ana kipato cha 5,000,000/= na ana deni la 10,000,000/=?. HAKUNA TOFAUTI.
Kufikiria kuwa madeni yako yatapungua utakapokuwa na pesa nyingi sio jambo la kweli na sio sahihi. Anza kujenga tabia bora kwa sasa ambazo zitakusaidia hata baada ya kuwa na pesa nyingi zaidi.
Usipokuwa mwangalifu kanuni ya Parkison's itakuathiri kama ambavyo tumejadili.
Nitakuwa makini na pesa zangu zikishakuwa nyingi.
Kuna watu wengi sana ambao huwa hawazingatii kabisa nidhamu ya pesa wanazopata kwani huwa wanaamini ni ndogo na hata wakizipoteza basi hazitakuwa na faida yoyote.
Kitu ambacho wanashindwa kuelewa ni kuwa pesa ndogo inayopotea leo, ikiendelea kupotea kwa miaka mingi inaweza kumaanisha upotevu wa pesa nyingi sana katika maisha yako.
Mfano tuseme kila siku mtu anafanya manunuzi yasiyo ya lazima ya dola 5 (2,300) ambayo inaweza kuonekana kuwa ni ndogo sana kwa wakati huo. Lakini hii kwa wiki inamaanisha ni dola 35 (80,997) na ni sawa na kupoteza dola 150 (347,130) kwa mwezi.
Pesa hiyo hiyo dola 150 kama ungeamua kuiwekeza kwenye uwekezaji ambao unatoa asilimia 10 kwa mwaka ungeweza kupata dola 30,727(Tsh 71,108,423)
Baada ya miaka kumi na kama ungeweka miaka thelathini ingekupa dola 339,073 (Tsh 784,682,736) na kwa miaka 40 ingekupa dola 948,611 (Tsh 2,195,275,576).
Hivyo unaweza kuona kuwa unapopoteza pesa kidogo kumbuka pia unapoteza fursa kubwa ya kifedha kwenye maisha yako.
Kama unataka kuwa na pesa nyingi kuliko ulizonazo kwa sasa itakulazimu kuwa makini na matumizi ya pesa zako.
SHERIA ZA FEDHA
“Pesa huwa zinaendeshwa na sheria zake maalumu na wale ambao wanazizingatia huwa wanafaidika sana na matokeo yake"
Lengo: Kukusaidia kujua sheria muhimu zinazoongoza pesa duniani kote.
UTANGULIZI
Moja ya jambo muhimu sana katika kuelekea mafanikio yako ya kifedha ni kujua kuwa fedha huwa zinaoongozwa na kanuni maalumu na kila ambaye huwa anazizingatia hizo kanuni huwa anafaidika nazo na kila ambaye huwa anazipuuzia basi huwa anapata madhara kutokana na kanuni hizo pia.
lla swali la kwanza na la muhimu ambalo unatakiwa kujiuliza ni kuwa Je, unazifahamu kanuni zenyewe?
Changamoto kubwa ya kwanza ambayo inawakabili watu wengi sana ni kuwa hawazijui kabisa kanuni zinazoongoza pesa na kwa sababu hiyo wamejikuta kuwa wanaathirika na kila wanapojaribu kufanya juhudi kuzipata ndivyo ambavyo huwa zinawaponyoka kabisa.
Sheria gani za fedha zimewasaidia watu wengi sana duniani?
Pamoja na ukweli kuwa kuna watu wengi sana ambao wamejitahidi sana kuandika juu ya sheria za fedha na namna ambavyo unaweza kufanikiwa kuna watu wawili ambao haswa ndio wanachukuliwa kama waanzilishi wa kanuni kabambe za kukusaidia kufanikiwa kifedha katika maisha yako.
Wa Kwanza ni George S.Clason aliyechapisha chapisho lake maarufu la kanuni 5 za dhahabu ambazo zimewasaidia watu wengi sana duniani kote.
Wa Pili ni Mike Phillips mtaalamu wa mambo ya benki kutoka nchini Marekani ambaye alichapisha makala yake ya sheria 7 za mambo ya fedha mwaka 1977.
Tuangalie sheria Tano Muhimu kwa leo.
Ingawa sheria zote hizi ni muhimu ila leo ningependa tujikite katika kanuni tano tukichukua kanuni baadhi toka kwa kila mmoja wa wataalamu niliowataja hapo juu.
Sheria ya Kwanza
Sheria ya kwanza kutoka kwa Phillips inasema kuwa pesa ni MATOKEO ya kufanya kitu ambacho watu wako tayari kukulipa kwani kinawapa faida fulani katika maisha yao.
Sheria hii inasisititza kuwa wakati wowote ule unapokuwa hauna pesa inamaanisha mambo yafuatayo:
Moja ni kuwa haujafanya kitu ambacho watu wako tayari kukulipa. Hii inakutaka uanze kufikiria kitu ambacho unaweza kuanza kukifanya abacho watu wako tayari kutumia pesa zao kukulipa bila kusita.
Pili unapokuwa umepungukiwa na pesa inaweza kumaanisha kuwa inawezekana unafanya kitu na uko bize lakini changamoto ni kuwa unachofanya watu hawako tayari kukulipa kabisa.
Hivyo kama leo umejigundua kuwa uko katika changamoto fulani ya maisha yako kifedha unatakiwa kujiuliza ni sababu ipi kati ya hizo mbili ambayo imekusababishia uwe hivyo ulivyo?
Naweza kufanya nini ambacho kwa sasa sikifanyi ili nivutie watu wanilipe pesa?
Sheria ya Pili
Sheria ya pili inatokana na Maandiko ya George Clason alliyesema kuwa fedha huongezeka kwa mtu ambaye anatafuta njia ya kuituma pesa yake ifanye kazi ya ya faida na imzalie kama mifugo.
Hii inamaanisha kuwa hautakiwi kuishia katika hatua ya kwanza tu ya kuweza kuhifadhi sehemu ya kipato chako katika akiba, unatakiwa uwe na uwezo wa kutumia kuwekeza sehemu ambayo inazalisha.
Hii haimaanishi utafute sehemu ambayo inazalisha kwa kiwango kikubwa, hata kama inazalisha kiwango kidogo sana ni bora kuliko kutozalisha kabisa.
Watu wengi huwa wanasubiri hadi wapate sehemu ambayo inazalisha sana ila wewe unaweza kuanza na sehemu ambayo inazalisha hata kama ni kidogo tu kwa sasa kulingana na uwezo wako.
Kulingana na kipato ambacho ninacho, ninaweza kuweka pesa zangu wapi ambapo zinaweza kuwa zinazalisha hata kwa kiwango kidogo kwa sasa?
Sheria ya Tatu
Sheria ya tatu inayotoka katika sheria 7 za Phillips inasema kuwa pesa huenda kwa wale ambao wanaamini kuwa pesa ziko kwa ajili yao.
Moja ya kitu ambacho kinawafanya watu wengi sana washindwe kupata fedha ni ile hali ya kutoamini kuwa wao wanaweza kupata pesa.
Sheria hii inakutaka kukabiliana na kila hali ya kutoamini kuwa una haki ya kupata utajiri wa kifedha (Naamini unakumbuka lecture yetu kuhusiana na Limiting belief).
Hivyo kwa ufupi ni kuwa kanuni hii inasema kuwa watu ambao wanapata pesa ni wale ambao wanazivutia pesa hizo kwa kuamini kwamba wanastahili kuwa nazo.
Kila ambaye haamini kuwa anaweza kupata pesa, basi pesa huwaa zinamkimbia kabisa na hawezi
kuzipata.
Swali kubwa na la muhimu kwako la kujiuliza ni kuwa, Je unaamini kuwa unaweza kupata pesa?
Sheria ya Nne
Sheria ya nne ambayo inatoka kwa Clyson inamfaa kila mtu wa kizazi chetu cha sasa, Sheria hii iansema pesa humkimbia mtu ambaye huilazimisha kupata kipato ambacho hakiwezekani au ambaye hufuata ushauri wa wajanja na walowezi au ambaye anaiwekeza kwenye sehemu ambazo hana ujuzi nazo na kwa kutaka kujifurahisha tu.
Nadhani hii ni moja ya kanuni ambayo inavunjwa sana na watu wa kizazi cha sasa na imesababisha watu wengi sana kupoteza fedha zao.
Kwa sasa kuna vitu vingi ambavyo vinavutia na vinawashawishi watu kuweka pesa zao kwa matumaini ya kupata pesa nyingi kwa wakati mmoja na kibaya zaidi ni kuwa wanakuwa hata hawajui namna ambavyo biashara hizo huwa zinafanya kazi.
Sheria mojawapo unayotakiwa kujiwekea ni kuhakikisha kuwa hauvutiwi tu na faida ya pesa inayoonekana kubwa isivyo kawaida bila kuchunguza kwa undani na kwa umakini.
Umeshawahi kusikia watu ambao walipoteza pesa au wewe mwenyewe kwa kukimbilia kuweka pesa zao mahali ambapo kulikuwa na matumaini ya kupata pesa nyingi sana kwa muda mfupi bila hata wewe/wao kuwa na ujuzi wa kujitosheleza katika biashara hizo?
Sheria ya Tano
Sheria ya 5 ambayo nayo ilisemwa na Clason nadhani ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu inasema. “Fedha huzidi kuongezeka, kumganda na kumlinda mtu ambaye anaiwekeza kama ambavyo huwa anashauriwa na wenye hekima katika kuitunza".
Moja ya kosa kubwa ambalo watu wengi huwa wanalifanya ni kuingiza fedha zao katika biashara na uwekezaji ambao kwanza hawana ujuzi nao kabisa lakini pili ni kuwa hawatafuti kabisa maarifa kwa watu ambao wana ujuzi wa kutosha.
Sheria ya mafanikio ya fedha inakutaka kwamba kila wakati unapotaka kutumia fedha zako kwa biashara ama uwekezaji wa namna yoyote ile ni lazima kwanza utafute watu ambao kwenye eneo hilo wana ujuzi na maarifa zaidi yako ili
wakupe ushauri na uzoefu wa kutosha.
Katika mipango yangu ya uwekezaji na biashara ninazotaka kufanya/ama ninazofanya ninapata ushauri kutoka kwa akina nani? See You At The Top
Kuishi juu ya maisha ya wastani inamaanisha ni uwezo wako wa kuweza kuvuka mstari muhimu ambao umewakwamisha watu wengi sana. Eneo muhim la mafanikio ya kifedha, linaanzia pale ambapo unapata maarifa muhimu na unaanza kuyaishi.
Kabla haujaweka kitabu hiki chini na kutangaza kuwa umekimaliza chote. Tafuta mahali ambapo utaandika mambo muhimu uliyojifunza na kisha hatua muhimu ambazo umedhamiria kuanza kuzichukua kama sehemu ya kufanyia kazi maarifa haya.
Kumbuka kuwa na ufahamu bila kuuweka katika vitendo, haitakusaidia kabisa.
Ukishamaliza kuweka mkakati na hatua ambazo utaanza kuzichukua ambazo zinaweza kuhusisha eneo lolote kati ya yale uliyojifunza, tafuta mtu ambaye utakuwa kila baada ya muda unashirikiana naye.
Ninaamini baada ya muda fulani utakuwa tayari unaishi kwenye mpango wako wa kifedha, umetengeneza nidhamu muhimu zinazohitajika na umejenga ufahamu sahihi juu ya mambo ya kifedha.
Haya yote yakitokea utakuwa umeshavuka mstari na umeanza kuishi maisha juu ya wastani. Usisahau kusoma makala zingine nilivyoviandika ili vikusaidie pia.
0 Comments