Maisha yanakunyuka utadhani uliwahi kumtukana shetani! Kumbe hata shetani mwenyewe humjui! Relax mpendwa! Hauko peke yako. Tuko wengi! Relax kabisaaaa maana kilio cha wengi harusi! Kikubwa tutiane moyo! Mimi leo naanza kukutia moyo!
Unalala chini sakafuni? Tena nguo zako ndio kama godoro na nyingine pazia? Halafu asubuhi ukiamka unavaa hizohizo kwenda kusaka maisha! Hapo hukumbuki kama ulikula ukashiba na leo huna uhakika wa kula. Umeishapiga watu mizinga hadi unajisikia aibu! Usiogope. Hiyo ni shule, hakikisha unatoka na Divisheni One kabisa! Baada ya dhiki faraja!
Unatamani kujiua kwa sababu dunia imekukazia utadhani inakudai? Usifanye hivyo! Ukijiua utaacha mkosi kwenye ukoo wenu. Kikubwa unapopata tatizo usiwaze ukubwa wa tatizo bali waza ukubwa wa Mungu katika hilo tatizo! Fanya hivyo maana Mungu hashindwi kitu. Mungu anaweza kufanya njia pasipo na njia, anaweza kufanya shibe pasipo na shibe na kufanya neema kwenye noma! Mungu ni Fire!
Mungu hawezi kukupa changamoto ya kukuzidi! Anakupa changamoto unazolingana nazo. Changamoto za Bill Gates hawezi kukupa wewe. Mwendo wa nyoka ni konakona lakini huwezi mkamata! Mungu akikupa ulemavu anakupa na muondoko wake. Ondoka hivyohivyo. We nenda tu hata kama utatembea kama lori limekata center bolt! Nenda utafika.
Unatamani kumkaba konda uondoke na hela anazokusanya kwa sababu tu huna hela? Usifanye hivyo maana hata yeye siyo hela zake! Ni hela za tajiri anayedaiwa mkopo benki. Unaona? Kila mtu ana shida zake! Pambana na hali yako, kikubwa usikae mbali na Mungu. Mungu yupo aisee. Tena anajibu kwa wakati zaidi ya haraka. Kikubwa usijichanganye.
Unajisikia kufakufa; moyo unataka kuchomoka kwa sababu umeachwa? Unafail sana ujue! Kwani wewe ndio wa kwanza kuachwa hadi utamani kunywa sumu ya panya ufe? La hasha! Wewe siyo wa kwanza kuachwa na wala hautakuwa wa mwisho kuachwa. Kikubwa tafuta mwingine kwa sababu mapenzi hayana ubaguzi ndiyo maana hata kichaa alibeba mimba! So relax! Habari za kipendaroho hula nyama mbichi ni ngano za kale!
Umelala kitandani uko hoi unaumwa hujiwezi? Usikate tamaa kwani kuna mwenzako muda huu amelala mochware, anasubiri kwenda kulala kaburini milele. Halafu amelala mochwari kwenye friji ameache gari la kifahari na kitanda chake cha kumi kwa kumi. Imagine atakuwa anajisikiaje huko! Ndiyo maana nakwambia jipe moyo utapona! Ukifa basi tena! Uzuri ukifa hutajua kama umekufa.
Kaza moyo ewe kiumbe, siku yako itafika utaachana na taabu za dunia. Utamu wa mua fundo, utamu wa maji kiu, utamu wa soda baridi joto; utamu wa nyama meno yagongane, kila kitu kina utamu wake; hata utamu wa kijiti nyama zikamate kwenye meno uchokonoe, loh! Kweli mke wa mwenzio usimfungie tai aliimba Remy Ongala! Sasa sijui tai ni nini!
Umepata hasara kwenye biashara yako? Usiifunge! Hasara ni moja ya vionjo vya biashara zilizofanikiwa. Hata mdada aliyekopa pesa anauza vitumbua ila faida ananunua kipodozi cha bei kubwa ajichubue kuutafuta uzungu kichaa! Mungu ana kazi nyieee! Ndiyo maana itikadi ya maskini wakati mwingine inakonga moyo. Itikadi ya ukipata kula, ukikosa mshukuru Mungu! Habari za kuweka akiba waachie wenye hofu ya maisha! Umaskini bana!
Maisha kama hayaendi nenda wewe tu mtakutana mbeleni. Mkipishana usilie maana kilio cha samaki hakina machozi. Yote hupelekwa na maji! Yakikupata bora usilie tu maana haitakusaidia kitu! Labda kutoa sumu mwilini! Maana baba zima kulia mbele za watu nacho ni kipaji. Halafu usipolia unawahi kufa! Ukilia unachekwa! Ni bora kulia uchelewa kufa kuliko kujikaza ukawahi kufa. Kifo hakina huruma.
Umefukuzwa kazi? Usijenge bifu na waliokufukuza! Uanaume ni kutafuta kazi nyingine; ukishindwa basi tengeneza kazi yako na wewe uwafukuze watakaozingua. Kumbuka mtegemea vya watu hufa maskini. Kumbe mshukuru aliyekufukuza kazi maana hakupenda ufe maskini. Amefanya kumpiga teke chura.
Kodi imekudhalilisha? Maana kuna jamaa alimuuliza mke wake mbona huyu mtoto amefanana na mwenye nyumba? Mke akasema tatizo hatujalipa kodi mume wangu. Yaani swali na jibu haviendani lakini vinakwenda pamoja! Haya maisha nyie yaacheni! Dunduliza tu upatapata vya kwako! Ni ngumu lakini utafanyaje sasa? Lakini ngumu haina maana haiwezekani.
0 Comments