Pale Unaposema Umekata Tamaa Hujui Namna Ulivyokuwa Karibu Kufanikiwa
Si rahisi kwa dereva kuona gari imemshinda basi na yeye kuamua kuacha gari iende itakavyo isipokuwa wengi hujitahidi kila wawezalo mpaka dakika ya mwisho na katika kufanya kila wanaloweza kufanya hujikuta wameweza kuepusha matatizo makubwa au kwa bahati nzuri wakanusurika vifo. Maisha nayo hufanania hali hizo kama ya dereva kuwa kuna wakati mambo unakutana nayo ni magumu na kuona mchezo utakushinda au kupoteza kabisa ila unapojipa muda wa subira, kuongeza juhudi kidogo basi unajikuta umeweza kuvuka na kushangaa namna ulivyovuka.
Subira ni muhimu katika nyakati ngumu, nyakati ambazo zinatia mashaka na nyakati ambazo mtu unajawa na wasiwasi mwingi. Subira huvuta heri katika kuishi maana wengi kwa kusubiri wameweza kupata vile ambavyo walifikiria wasingevipata. Haja ya kungoja na kuweka subira mambo yanapokuwa yameenda tofauti na vile usivyotarajia kunahitajika mno kwa zama tuishizo ili usijekupoteza hata kile kidogo ulichokuwa nacho.
Mambo katika maisha hubadilika pale ambapo licha moyo hujawa na wasiwasi, kusita sita kwingi bado mtu akiweka jitihada, moyo wa ujasiri nafasi ya kuvuka huwa ni kubwa. Watu hushindwa kupata vile ambavyo walitamani kuvipata sababu mambo yalipokuwa magumu waliamua kusalimu amri mapema na wako tayari kuaga mchezo huo. Utakuwa umekutana na watu kwa mambo kuwa magumu wameshajikatia tamaa na kusema huenda ninalopigania si fungu langu. Magumu yanayokuwa mengi na hayana majibu ni rahisi mtu kuona hapa siwezi kuvuka, hapa sina ujanja na mtu hukubali kushindwa.
Endelea kidogo katika unachokipambania, usiwe mwepesi kuacha sababu ya ugumu, usikubali kuacha kuendelea na safari sababu huoni dalili za kufanikiwa. Kuna wakati mwingine asili inampitisha mtu katika magumu ili kupima ni kiasi gani amejitoa kukitaka hicho kitu. Ikitokea umeng’ang’ana vya kutosha basi asili huwa haina jinsi ikunyime nafasi ya hicho kitu. Wale watu ambao wapo tayari kuwa ving’ang’anizi hadi mwisho ndio wana nafasi ya kupata na kufanikiwa.
Unapofika wakati ambao unajiona umeishiwa nguvu katika kupambana na kile unachotaka kitokee basi jipe nafasi ya kujaribu tena kwa mara nyingine. Jipe nafasi ya kusema nitajaribu tena na usikubali kuacha kabisa kujaribu. Ni heri ujipe mapumziko kidogo ila sio kuacha kuendelea mbele sababu ya magumu.
0 Comments