Muhtasari
Irritable bowel syndrome (IBS) ni hali ya muda mrefu inayoathiri utumbo mkubwa (koloni). IBS ni hali ya kawaida sana, hasa kwa watu wenye umri mdogo na wanawake. Sababu za hali hii kutokea hazieleweki vizuri, lakini mfadhaiko na kuathirika kirahisi na vyakula fulani huweza kuchangia. Dalili kuu ni maumivu ya tumbo, tumbo kujaa gesi na kuharisha au kufunga choo. Ni muhimu kwa daktari kuhakikisha dalili hizi hazisababishwi na ugonjwa mwingine kabla ya kufanya utambuzi wa IBS. Ingawa hamna tiba maalum ya hali hii, mabadiliko katika mienendo ya maisha na lishe mara nyingi husaidia kupunguza dalili.
Hatari
Wanawake huathirika zaidi na irritable bowel syndrome kuliko wanaume. Hali hii hutambuliwa zaidi kwa vijana, ingawa inaweza kumathiri mtu mwenye umri wowote. Sababu za irritable bowel syndrome kutokea hazieleweki kikamilifu, lakini mfadhaiko na kuathirika kirahisi na vyakula fulani huweza kuchangia.
Matibabu
Hamna matibabu maalum yanayolenga chanzo cha irritable bowel syndrome, lakini kuna vitu vingi vinavyoweza kusaidia kupunguza dalili. Kuepuka vyakula vinavyochochea dalili huweza kusaidia watu wengi wenye hali hii. Hii hujumuisha (miongoni mwa mengine) vyakula vinavyoongeza gesi (brokoli, kabichi, maharage), vyakula vyenye mafuta na vyakula vyenye kafeini. Watu wengi huona kuwa kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia. Mfadhaiko unaweza kusababisha dalili, na kujifunza jinsi ya kudhibiti mfadhaiko huweza kusaidia baadhi ya watu. Dawa huweza kusaidia kufunga choo (constipation) au kuharisha.
Ubashiri
Ingawa hali hii haina na tiba, watu wengi hujifunza kuzidhibiti dalili zao na huona kuwa dalili zinapungua kadri muda unavyoenda. Watu wengi hawapati madhara ya muda mrefu kutokana na hali hii.
Dalili
Dalili za irritable bowel syndrome zinaweza kutofautiana sana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Dalili kuu ni maumivu ya tumbo, tumbo kujaa gesi, kujamba, kuharisha au kutopata choo na kamasi katika kinyesi. Dalili zinaweza kupungua baada ya kujisaidia haja kubwa. Mfadhaiko au vyakula fulani huweza kusababisha dalili kutokea. Vyakula vinavyochochea hali hii vinaweza kutofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Utambuzi
Utambuzi hufanywa na daktari kulingana na dalili na uchunguzi wa kimwili. Ni muhimu kwa daktari kuhakikisha dalili hizi hazisababishwi na ugonjwa mwingine kabla ya kufanya utambuzi wa IBS, na hii huweza kuhusisha kufanya vipimo. Watu wanaweza kuambiwa kuweka shajara ya vyakula wanavyokula ili kuona kama kuna vyakula vyovyote vinavyofanya dalili kuwa mbaya zaidi. Kipimo ambacho kamera ndefu hupitishwakwenye kinywa au njia ya haja kubwa ili kuangalia tumbo na utumbo (gastrointestinal endoscopu) huweza kufanywa ili kutofautisha ugonjwa huu na magonjwa mengine yanayosababisha dalili hizi. Vipimo vingine vinaweza kujumuisha vipimo vya damu, vipimo vya pumzi vya laktosi, X-rays au CT scan.
0 Comments